29 Mei 2025 - 17:31
JMAT Yatoa Wito kwa Viongozi wa Dini Nchini Kenya wa Kushirikiana Katika Kuwaongoza Wananchi wao ili Kuheshimiana na Kutunza Mahusiano ya Amani

Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum: "Wakenya ni ndugu wa Watanzania, na mbali na uhusiano wa kijamii, ni ndugu wa damu. Tunatambua kuwa mizozo hii inahusu zaidi vijana wa Kenya, lakini ni muhimu kuwakumbusha kuwa heshima ni nguzo muhimu katika mahusiano ya mataifa. Tunaamini Kenya ina Viongozi wa Dini na Serikali wanaoweza kusaidia katika hili."

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlu-Bayt (as) - ABNA- Dar es Salaam, Tanzania – Uongozi wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) umeomba ushirikiano wa karibu na viongozi wa Dini nchini Kenya katika kuwaongoza na kuwashauri wananchi wao kuheshimiana na kudumisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya mataifa hayo mawili.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa JMAT-TAIFA, Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuhusu tamko la Jumuiya hiyo kuhusu mizozo ya matusi na uvunjifu wa maadili baina ya baadhi ya vijana wa nchi hizi mbili.

Sheikh Dkt. Alhad amesema:
"Wakenya ni ndugu wa Watanzania, na mbali na uhusiano wa kijamii, ni ndugu wa damu. Tunatambua kuwa mizozo hii inahusu zaidi vijana wa Kenya, lakini ni muhimu kuwakumbusha kuwa heshima ni nguzo muhimu katika mahusiano ya mataifa. Tunaamini Kenya ina viongozi wa Dini na Serikali wanaoweza kusaidia katika hili."

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuenzi heshima za viongozi wa mataifa jirani, akifafanua: "Tunaomba viongozi wetu wa Kenya wawasihi vijana wao kuonyesha heshima kwa viongozi wa taifa jingine, ikiwa ni pamoja na viongozi wa Tanzania. Heshima kwa taifa lolote ni msingi wa maadili ya watu wake."

Sheikh Dkt. Alhad pia alionya dhidi ya matusi na vitendo vya utovu wa adabu vinavyoelekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na wananchi wa Tanzania, akasema:
"Iwapo matusi haya yataendelea, itakuwa ni dhihirisho la kumkosea Mwenyezi Mungu kwa kuwatukanisha Wazazi wao na kupoteza heshima na ustaarabu katika uso wa dunia."

JMAT inaamini ushirikiano baina ya viongozi wa dini ni muhimu sana katika kudumisha Amani, Maridhiano, na Mshikamano wa kiafrika kati ya Wananchi wa Kenya na Tanzania.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha